Halmashauri ya wilaya ya Kibaha inaendesha kampeni ya siku 7 ya utoaji wa chanjo ya Uviko-19 kwa watu wote wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea iliyoanza tarehe 25/11/2022 hadi tarehe 30/11/2022, pamoja na chanjo ya ugonjwa wa Polio kwa watoto wenye umri kuanzia 0 hadi miaka 4 kampeni ya chanjo ya polio itaanza tarehe 1/12/2022 hadi tarehe 4/12/2022.
Katibu Tawala Wilaya ya Kibaha Sozy Ngate amesema Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya njema hivyo Wilaya ya Kibaha kwa pamoja imejipanga kuhakikisha inafikisha asilimia 100 ya chanjo ya UVIKO kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha kwa kuendelea kutoa elimu na kufanya uhamasishaji wa kutosha.
Katibu Tawala ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa kamati ya msingi ya Afya ngazi ya jamii (PHC)yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo kuhusu chanjo ya Uviko 19 na chanjo ya polio.
Aidha Sozy amewataka wazazi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ya polio kwani chanjo hii inatolewa ili kuwapa uimara watoto wao katika kujikinga na ugonjwa wa polio ambao hauna tiba na baadhi ya madhara ya ugonjwa huu ni pamoja na kuleta athari katika mfumo wa fahamu wa mtoto na kupooza. Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha watoto wote wanakuwa salama kiafya ndo maana kuna chanjo ya polio ambapo mtoto anapewa matone ya chanjo.
“ Katika kuhakikisha tunakamilisha lengo la kutoa chanjo kwa walengwa 18,525 ndani ya muda wa siku nne za Kampeni yaani tarehe 01/12 - 04/12/2022. Tumekubaliana kwa pamoja kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo ya polio na madhara yanayoweza kujitokeza kwa mtoto asiyepatiwa chanjo hiyo. Hivyo tuna imani tukishirikiana kwa pamoja tutafanikisha kwani toka awamu zilizopita za chanjo Halmashauri ya Wilaya Kibaha tulifanya vizuri”. Amesema Ngate
Mratibu wa chanjo halamshauri ya wilaya kibaha Khadija Telacky amewataka wananchi kuchanja chanjo ya uviko 19 kwani haina madhara na itwakinga na ugonjwa wa uviko 19 pia amewataka wazazi kuwapa ushirikiano wa kutosha wahudumu wa afya watakaopita kwenye nyumba zao na mitaa kwa kuwatoa watoto wote wenye umri kuanzia miaka0-4 ili waweze kupata chanjo ya polio kwani ugonjwa wa polio ni ugonjwa hatari .
Telacky amesema mpaka sasa kwa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha wameshachanja chanjo ya Uviko kwa asilimia 77 wanategemea kumaliza asilimia 33 zilizobaki ifikapo desemba 2022.
Pia mratibu huyo wa chanjo ameitaka kamati ya msingi ya afya kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa jamii kuhusu chanjo ya uviko na polio
Mchungaji Chamade Horohoro ameahidi atakuwa balozi mzuri wa kuelimisha waumini umuhimu wa chanjo kwani binadamu anahitaji mambo matatu kwa ajili ya ustawi wake ambayo ni afya ya akili, utimamu wa mwili na uelewa sahihi hivyo akikosa kimojawapo atakuwa na mapungufu ndio maana nahamasisha jamii kuchanja ili wawe na utimamu wa mwili
KIBAHA DISTRICT COUNCIL
Anwani ya Posta: P.O BOX 30153
Simu ya Mezani: +255 23240224
Simu: +255 0767520048
Barua pepe: ded.kibaha@pwani.go.tz
Copyright ©2017 Kibaha District Council . All rights reserved.